Huu ni mwendelezo wa chapisho la 48 Laws of Power ambalo ni utambulisho wa makala mfululizo kuhusu kitabu hiki ambacho ni maarufu sana duniani kote kuhusu sheria za kupata nguvu na mamlaka. Kila makala ya muendelezo itahusisha walau sheria tatu (03) katika sheria 48 zilizo kwenye kitabu hiki.
Karibu MAISHA MAX ambapo kuna mengi ya kujifunza na kukuwezesha kupata MAARIFA, kuimarisha AFYA pamoja na kujiwezesha kwenye UCHUMI binafsi. Pia tunapatikana katika mitandao ya kijamii; X 'twitter', Facebook, Tiktok, Youtube, Instagram, Telegram.
Sheria ya 4: Always say less than necessary (Kila mara jizuie kuongea maneno mengi)
- Kutokuwa dhahiri sana na kujiwekea hali ya utata kuna nafasi ya kuwavutia watu.
- Unavyozidi kuongea basi ndio nafasi ya kuropoka yasiyofaa pia inaongezeka, na maneno ni kama maji tu yakishamwagika hayazoleki.
- Unavyozungumza machache, basi unawapa nafasi wengine kuongea zaidi yako na ukiwa makini hiyo itakufungulia zaidi nia na siri zao ambazo huenda wamezificha
Mfano
Mfalme LOUIS XIV alikuwa akisikiliza kwa umakini hoja alizoletewa na mawaziri wake, na hakuna hata mmoja aliyejua mfalme anafikiria nini katika wakati husika. Kila wakimletea habari alikuwa akisema "sawa nitaliangalia" hakujali kujadiliana nao wala kuwapatia majibu papo hapo. Hali hii ilimfanya kila mmoja awe na hofu juu ya anachofikiri mfalme.
Kinyume cha Sheria hii
Ukimya kuna muda unaweza kufanya watu wakudhanie vibaya, au unaweza ukasema kauli fupi ila imejaa utata, hivyo ni vyema kuhakikisha umeweka sawa kauli zako na kujua ni nani unazungumza naye katika wakati husika.
Sheria ya 5: So much depends on reputation - Guard it with your life (Wasifu wako ni muhimu sana - Ulinde hata kwa kuweka maisha yako rehani)
- Linda na utunze wasifu wako.
- Watu wanaokuzunguka pamoja na dunia nzima wanaangalia sifa zako njema kama kipimo cha wewe ni mtu wa aina gani.
- Sifa njema ni kama wakala ambaye anakutambulisha kwenye fursa.
- Chagua sifa moja ambayo utadumu nayo maisha yako yote.
- Kama kuna namna umeharibu wasifu wako kwa kujihusisha na sifa mbaya, basi tafuta mtu ambaye ana wasifu mzuri awe rafiki yako.
- Pambana na adui zao kwa kuwachafulia sifa zao.
- Mtu akikuzidi nguvu, njia mojawapo ya mashambulizi ni kumchafulia sifa zake nzuri.
- Umakini unahitajika kwa maana kibao kinaweza kukugeukia na ukaonekana mtu wa ajabu sana kwa kutumia mbinu chafu kama hii.
Kinyume cha Sheria hii
Hakuna kinyume cha sheria hii, ni muhimu sana kulinda sifa zako nzuri na wasifu wako kiujumla hata ikibidi kutofautiana na watu.
Sheria ya 6: Court attention at all costs (Vuta macho ya watu kwa gharama yoyote)
- Uwezo wa kuvuta macho ya watu kwa ustadi unaweza kukuwezesha kufungua milango mingi ya fursa.
- Rasilimali adimu sana duniani ni uwezo wa kuwavutia watu watambua uwepo wako au laah watambue kazi yako.
- Tumia njia mbalimbali kwenye kusaka "attention" kama itakubidi tafuta wazo ambalo wengi wanakubaliana nalo na nenda kinyume nalo, sambamba na mbinu nyingine nyingi.
- Tengeneza taswira ya utata
- Utata unawavutia watu, kwa maana inabidi watumie nguvu kukujua zaidi.
- Si lazima ufanye mambo makubwa sana kutengeneza utata, kukaa kimya kwa muda, kupotea kwenye ramani au kufanya vitu ambavyo havikutarajiwa na watu kila baada ya mda fulani kutawafanya watu watengeneze taswira kukuhusu ambayo huja na heshima na nguvu dhidi yao.
Kinyume cha Sheria hii
Kuna namna kadhaa sheria hii inaweza kwenda tofauti na matarajio;
- Ni vizuri kubadilisha njia zako mara kwa mara, mazoea kutoka kwa watu yanaweza kukupotezea lengo lako kikamilifu.
- Taswira ya utata ambayo utaitengeneza, hakikisha haitafsiriwi kwamba wewe una tabia za udanganyifu.
- Kuna wakati, kutafuta sana "attention" kunaweza kukuletea kashfa mbaya ambazo zitaharibu wasifu wako (Sheria ya 5). Kuwa na kiasi kwa kufahamu ni wapi uchore mstari.
- Ukitafuta sana "attention" kuna uwezekano mkubwa wa kuonekana hujiamini na watu wakachukizwa na mienendo yako.
0 Maoni