Je, ulijifunza kuhusu pesa shuleni?
Je, wazazi wako walikufundisha kuhusu pesa?
Video ya leo itakuwa mwongozo wa mwanzo kabisa juu ya elimu ya kifedha, kwa hivyo ikiwa unataka kujua jinsi ya kutumia pesa vizuri kwa kufanya maamuzi bora ya kifedha na mwisho kuishi maisha mazuri zaidi na kufikia malengo yako yote ya kifedha, hakikisha unatazama video hii hadi mwisho na usisahau kuLIKE, kuCOMMENT na la muhimu zaidi ni kuSUBSCRIBE ili usipitwe na video zetu mpya.
Mataifa ya dunia ya kwanza kama vile Marekani, Canada n.k yana mwezi maalumu wa kuazimisha umuhimu wa elimu ya kifedha tofauti na mataifa ambayo bado hayajaendelea, lakini pia utafiti uliofanywa na WORLD ECONOMIC FORUM ukihusisha dunia nzima, ulibaini kuwa mtu mmoja kati ya watatu ndio ana elimu kuhusu fedha, hii takwimu sio nzuri sababu kuna maamuzi mengi ya kifedha ambayo hayaepukiki katika maisha yetu ya kila siku. Na katika makundi ya umri, kundi la vijana ndio ambalo lina hatari kubwa ya kufanya maamuzi yenye athari zaidi kwenye mustakabali wao binafsi lakini pia mustakabali wa jamii na taifa kwa ujumla, kuna haja ya vijana kujielimisha kuhusu fedha sababu ndio wazazi na viongozi wa kesho. Kwa kusema hivyo, wacha tuanze makala hii.
Elimu ya kifedha ni nini? Elimu ya kifedha ni uwezo wa kufanya maamuzi ya kifedha ya busara ambayo yanakusaidia kufikia mtindo wa maisha unaotaka. Elimu hii inajumuisha hasa kujipatia kipato, kupanga bajeti, kukopa pamoja na kulipa deni ama madeni, kuweka akiba, kuwekeza, kujilinda kifedha na kwa ujumla ni kusimamia fedha zako.
Kwa nini elimu ya kifedha ni muhimu sana? Kadri unavyokuwa na elimu kuhusu fedha, ndivyo unavyofanya maamuzi bora zaidi na fedha zako, na kwa kuwa fedha ni kitu adimu hatuna budi kujielimisha ili kuimarisha usimamizi wa fedha zetu. Unaweza kuwa na kazi inayolipa zaidi dunia nzima na bado ukaishiwa pesa kwa kushindwa kuzitunza. Kwa sababu tu unapata pesa nyingi labda kama mshahara haikufanyi kuwa bora katika kuzisimamia. Hivyohivyo unaweza kuwa na kazi inayolipa kidogo lakini bado ukaweza kujenga utajiri kwa sababu una ujuzi mzuri wa usimamizi wa pesa. Bila elimu ya kifedha, pesa hupotea. Hata wahenga walisema mali bila daftari, hupotea bila habari, hapa natamani kuamini kwamba daftari ilikuwa na maana ya elimu ya kifedha. Kama haipo hii inamaanisha utafanya kazi zaidi, utapoteza muda mwingi zaidi na itakuwa ngumu kwako kutengeneza utajiri.
Je hautaki kuwa na uwezo wa kumudu kununua vitu vizuri kwenye maisha yako ? Vipi kuhusu kusafiri, kununua nyumba, kuwa na watoto, ama gari la ndoto yako? Je, utakuwa na pesa za kutosha unapostaafu? Na hapo ndipo elimu ya kifedha inapoingia, ukiwa nayo basi itakusaidia kukaribia malengo yako ya kifedha. Je, una uwezo wa kumudu gharama za dharura ? Unapojua jinsi ya kusimamia pesa zako, gharama za dharura zinaweza pia zisikupe tabu.
Sasa tuangalie, pesa hufanya kazi vipi? Pesa ni malipo yanayokubalika kwa bidhaa ama huduma. Unapofanya kazi, inamaanisha unatoa bidhaa au huduma. Kwa watu wengi, kufanya kazi kunachukua muda wao wote, kwa hivyo kimsingi wanabadilisha muda wao kwa pesa. Unaweza kutengeneza pesa kibao lakini bado tuna mipaka kwenye muda wetu hapa duniani. Kwa hivyo, kwa nini watu wengi hawana ufanisi na pesa zao? Ni kwa sababu hawana elimu ya kifedha.
Tukianza na kupata kipato. Kupata kipato ni msingi wa fedha zako binafsi. Hizi ni pesa zinazoingia mfukoni kwako. Aina za mapato ni pamoja na mshahara wa kibarua (Kwa maana malipo kulingana na masaa ya kazi), mshahara wa mwezi, kamisheni, bonasi. Unapofikiria kuhusu kazi au taaluma, unapaswa pia kuzingatia mtindo wa maisha unaotaka kuishi na je, utapata pesa za kutosha kumudu mtindo huo wa maisha. Unapaswa pia kuzingatia faida unazoweza kupata kama vile pensheni, bima za wafanyakazi, faida za umoja wa wafanyakazi n,k. Lakini pia nafasi ya kupanda ngazi zaidi ipo ? Je, hii kazi au fani ina sokoi? Je, kuna ugumu au urahisi kiasi gani kupata kazi? Je, utahitaji kupata mkopo wa elimu ili kusomea hiyo kazi? Na mwisho, je, kazi hii ni kitu ambacho ungependa kufanya au unapenda tu pesa?
Kwa kuwa kupata mapato ni msingi wa fedha zako binafsi, msingi wako ukiwa bora, sehemu nyingine za fedha zako binafsi zitakuwa rahisi zaidi. Lakini usijizuie tu kwa kuwa na chanzo kimoja cha mapato. Ikiwa unataka kweli kuongeza pesa zinazoingia mfukoni kwako, zingatia vyanzo vingine. Kuna aina saba tofauti za vyanzo vya mapato unavyopaswa kujua: mapato ya mshahara, mapato ya faida, mapato ya riba, mapato ya gawio, mapato ya kodi, mapato ya faida ya mtaji, na mapato ya mrabahai.
Mapato ya mshahara ama kazi ndiyo yanayofahamika na wengi, na ndio chanzo kikuu lakini aina hii ya mapato inategemea kiwango cha ujuzi ulio nao pamoja na muda unaotumia kila siku kuifanya hiyo kazi. Pia kuna mapato ya faida, haya yanapatikana pale unapouza bidhaa au huduma kwa fedha zaidi ya uliyotumia katika kutengeneza bidhaa au huduma hiyo, kwa maana umepata faida, hapa wanaingia wafanyabiashara na wajasiriamali na aina hii ya mapato inaweza kukuzwa endapo utafanya mauzo zaidi, lakini kuna kiwango flani cha hatari ambacho kinaingia hapa sababu lazima uwekeze kidogo. Aina nyingine ya mapato ni mapato ya riba ambayo utapata endapo umeweka pesa zako mfano kwenye savings account, lakini kipato hiki kinahitaji mtaji mkubwa sana ili upate faida inayoeleweka, na upande wa hatari (risk) ni almost hakuna na ni kama utatengeneza pesa huku umelala, pia kuna mapato ya gawio na ni aina ya mapato ambayo hupatikana endapo unamiliki hisa za kampuni fulani ambayo hutoa gawio kwa wanahisa wake, mara nyingi ni kila robo mwaka au nusu mwaka, aina inayofuatia ni mapato ya kodi ambayo hupatikana kwa pale unapokodisha mali yako itumike na mtu ambaye atakulipa, inaweza kuwa ni kodi ya nyumba, kodi ya gari, kodi ya vifaa n.k. Aina inayofuatia ni mapato ya faida ya mtaji ambayo hupatikana pale utakaponunua katika bei ya chini na kuuza katika bei ya juu mifano hapa ni soko la hisa endapo unamiliki hisa na utafanya uamuzi wa kuuza hisa zako zinapopanda thamani, au inaweza kuwa ni ununuzi wa wali isiyohamishika kama vile nyuma ambayo utaiuza kwa bei ya juu baada ya kufanya ukarabati, kipato cha aina hii ni maarufu pia. Na mwisho kuna mapato ya mrabaha ambayo hupatikana pale utakaporuhusu mali yako isiyohamishika kumilikiwa na wengine baada ya kukulipa, hii inaweza kuwa kama hakimiliki ya kazi za sanaa, leseni au rasilimali ambayo unaimiliki.
Kuna muda mdogo tu kwenye siku, ikiwa unataka kweli kuongeza mapato yako, utahitaji vyanzo vya mapato vinavyolipa zaidi na vinavyohitaji muda mdogo. Na hii itakufikisha kwenye hali ya kutengeneza fedha hata kama umelala.
Mapato haya yote yamebeba sura ya kuwekeza. Uwekezaji kwenye biashara inayoweza kukulipa mapato ya faida, uwekezaji katika mali isiyohamishika inayoweza kukulipa mapato ya kodi au faida ya mtaji, ama uwekezaji katika soko la hisa ambao utaweza kukulipa mapato ya gawio na pia faida ya mtaji.
Sehemu moja muhimu ya elimu ya kifedha ni uwekezaji. Moja ya njia rahisi za kuwekeza ni katika soko la hisa. Hapa ndipo utajiri mwingi umejengwa kwa faida ya mtaji, mapato ya gawio na mchanganyiko. Mfano Tanzania tuna Dar-es-Salaam Stock Exchange (DSE) ambayo ina makampuni mbalimbali ya kiTanzania na thamani ya hisa zao pamoja na gawio, lakini kiukweli hisa za Tanzania hazina upepo sana kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo kusuasua kwa uchumi wetu, ila ni eneo ambalo mtu unaweza kulifanyia utafiti zaidi kwa maana hisa si lazima ununue za Tanzania tu, teknolojia inatuwezesha kununua hisa hata za makampuni ya kimataifa, na unaweza kujifanyia mwenyewe au kutumia dalali.
Uwekezaji wa kujifanyia mwenyewe ni wakati unafungua akaunti ya udalali na kufanya uwekezaji mwenyewe. Kabla ya kuchagua kampuni ya udalali ya kutumia, fikiria kwa kina wewe ni aina gani ya mwekezaji kama ni: mwekezaji wamuda mrefu, mwekezaji wa kutegemea gawio peke yake, lakini pia Masoko gani unataka kuwekeza: soko la Marekani, soko la Kanada, la kimataifa? Na tafuta elimu zaidi kuhusu uwekezaji huu wa hisa, nitoe tahahari kwamba kwa njia yoyote ile video hii isihusishwe endapo utafanya maamuzi kuhusu uwekezaji wa hisa kwa kukurupuka, fanya maamuzi at your own risk.
Teknolojia imeenda mbali zaidi hadi kuhusisha roboti kwenye uwekezaji huu wa hisa, ambacho wewe unachopaswa kufanya ni kuainisha tu kiwango chako cha uvumilivu, kiasi cha mtaji wako, kiasi unachoweza kuwekeza kila inapohitajika n.k
Ukishafikia lengo lako, toa pesa zako na seti lengo jipya. Labda lengo lako ni kuanza kuwekeza katika mali isiyohamishika. Aina hii ya uwekezaji inahitaji pesa nyingi zaidi, kawaida ni angalau asilimia 20 ya bei ya ununuzi kwa maana labda unaweza kukopeshwa kwa bei hiyo. Katika mali isiyohamishika mfano nyumba, unaweza kukuza pesa zako kwa njia tofauti. Unaweza kukodisha mali yako kwa rehani na kupata faida ya ile tofauti ya kununulia na kupangisha na wakati unafanya hivyo thamani ya nyumba yako pia inaongezeka. Au unaweza kununua mali na kufanya ukarabati na kuuza kwa bei ya juu. Inaonekana rahisi kwa kusema tu lakini kuna mengi ya kujifunza kuhusu aina hii ya uwekezaji na utahitaji timu ya wataalamu ili kusaidia kufanikisha hilo kama wasimamizi wa mali, wakandarasi wa ujenzi, madalali, wanasheria na wakala wa mikopo. Ikiwa uko tayari kuanza na aina hii ya uwekezaji, kuna sehemu nyingi za bure za mtandaoni ambazo unaweza kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji kwenye mali isiyohamishika.
Lakini pia unaweza kufanya uwekezaji kwenye biashara yako binafsi au ya mtu mwingine, na hapa ni lazima ufanye utafiti ili kufahamu ni aina gani ya biashara unahitaji kufanya, je itahusisha uuzaji wa bidhaa ama utoaji wa huduma ? Ni bidhaa au huduma gani zitakurudishia faida kwenye uwekezaji wako ? Je kuna faida kwenye hiyo biashara ? Utahitaji kuwa na Business Plan (Mpango wa Biashara), na mwanzoni ni lazima uweke mtaji wako mwenyewe walau ndani ya miaka miwili kabla ya kutafuta wawekezaji wa nje waje kutia nguvu, sambamba na hilo bila kusahau usajili wa biashara yako kwenye mamlaka husika, na watu gani utafanya nao kazi ni muhimu sana kufanya kazi na watu makini, umakini na uchapaji kazi ndio uwe kigezo cha kwanza hakikisha haufanyi kazi na watu kwa kigezo cha urafiki au undugu, labda tu kama kweli wana kigezo cha kuwa wachapakazi na hodari kwenye sekta au fani husika.
Mpaka kufikia hapa, tumegusia suala la kuingiza kipato kwa juu juu, ni ngumu kumaliza kila kitu ndani ya muda mfupi huu wa video hii, lakini usisahau kuSUBSCRIBE kwenye channel hii ili usipitwe na video nyingine nyingi kuhusu eneo hili la kuimarisha uchumi binafsi pamoja na elimu ya kifedha.
0 Maoni