Hii ni makala fupi kuhusu filosofia ya ustoiki na mwisho huenda utafikia hitimisho kama unaihitaji walau kidogo katika maisha yako, kwa sababu watu hawaisemi mara nyingi lakini hapa nitawaambia kuhusu falsafa hii ya ustoiki. Ustoiki ulikuwa falsafa iliyostawi kwa miaka 480 katika Ugiriki na Roma ya kale na ulikuwa maarufu kwa kila mtu kutoka kwa watumwa hadi kwa matajiri kwa sababu tofauti na falsafa nyingine, ustoiki ilikuwa msaada. Ilisaidia wakati tunapopatwa na hofu, tunapotaka kukata tamaa, kuwa na hasira juu ya maisha yetu. Tunaiheshimu falsafa hii na tunawapachika watu majasiri huenda kwa kujua au kutokujua.
Kuna wanafalsafa wawili wakuu wa Ustoiki. Wa kwanza ni mwandishi wa Kirumi na mwalimu wa Mfalme Nero, alikuwa akiitwa Seneca. Aliishi kati ya mwaka 4 AD na 65 AD. Ndiyo, Seneca alikuwa mwalimu wa Nero, yule dikteta maarufu ambaye alilala na mama yake mwenyewe, kuwabaka wavulana wadogo na pia alimuamuru mwalimu wake Seneca ajiue mbele ya familia yake mwenyewe kwa sababu tu alitamani kufanya hivyo.
Na mtu wetu mwingine katika Ustoiki ni Mfalme Mkarimu na Mwerevu wa Kirumi, Marcus Aurelius, aliyeishi kati ya mwaka 121AD na 180 AD. Alilazimika kutumia sehemu kubwa ya utawala wake kwenye mipaka ya himaya yake akipambana na makabila ya Wajerumani walioshindikana, lakini alipata muda wa kuandika moja ya kazi kubwa za falsafa kuwahi kutokea, kitabu kinachoitwa "Meditations," wakati wa usiku kwenye hema lake kipindi hiko cha vita.
Kuna matatizo mawili makuu ambayo falsafa ya Ustoiki inaweza kutusaidia, hasa la kwanza ni wasiwasi. Wakati unahisi wasiwasi kuhusu kitu, watu wengi hukukasirisha kwa kuamini ni wajibu wao kukufurahisha. Hata kama wana uelewa kiasi gani, watasema mambo kama "itakuwa sawa," "usijali," hata "furahi” “kila kitu kitakuwa poa”. Wastoiki hawakupendezwa na hii,.walichukia aina yoyote ya faraja inayolenga kumpa msikilizaji “matumaini”. Matumaini ni opiamu (kama madawa ya kulevya) ya hisia na lazima yakomeshwe kabisa kwa mtu kuwa na nafasi yoyote ya amani ya ndani. Na kwenye falsafa hii ya ustoiki, matumaini inaaminika yanakuinua juu sanaa na hatimaye yanakuporomosha kutoka kwenye hicho kilele, bila kutimiza azma na haja zako za suluhisho na amani ya kweli.
Wastoiki wanashauri kuchukua njia tofauti. Kupata utulivu, mtu lazima ajisemee kitu tofauti kabisa na kujipa matumaini, ajiweke kwenye giza: kwa kauli kama “itakuwa mbaya” “naweza kulazimika kwenda gerezani” “pengine nitafukuzwa kazi na kuaibishwa” “rafiki zangu karibu wote watafanikiwa”. Lakini stoiki anakuwa na imani kwamba kila kitu kitakuwa sawa pasi na kujipa matumaini ya uongo na inatuimarisha na jambo lolote baya linaloweza kutokea sababu kila mmoja wetu ana nguvu zaidi kuliko tunavyodhani. Na mwisho ukiona ngoma inakuwa ngumu sana stoiki anaweza mpaka kujifowadi kwa Sir God, ila hapa binafsi ninapingana na falsafa hii mfano kama Marcus Aurelius alisema, je huoni njia ya uhuru mbele yako, ni simple tu unatakiwa ugeuze viganja vyako (akimaanisha njia ya kujikata mishipa ya kiganjani ambayo ndio ilipelekea kifo chake baada ya kuamuriwa na mwanafunzi wake Mfalme Nero). Ni kweli ukitupwa gerezani haitakuwa raha, wala ukipoteza kazi au kufanywa kichekesho mbele ya watu, lakini mtu atavuka. Ustoiki hututia moyo dhidi ya mabaya zaidi ambayo hatima ya maisha inaweza kuturushia.
Ili kujenga picha ya uvumilivu wa mtu mwenyewe, ustoiki unapendekeza mtu afanye mazoezi mara kwa mara ya kujiweka kwenye hali mbaya zaidi. Kwa mfano, mara mbili kwa mwaka mtu anapaswa kuvua mavazi yake maridadi na kuvaa vitambaa vichafu, kulala kwenye sakafu ya jikoni ama kula tu mkate mkavu na maji ya mvua kutoka kwenye bakuli la mnyama wake. Kwa kufanya hivyo, utagundua jambo la kushangaza kama Marcus Aurelius alivyoandika: kwamba ili kupata maisha ya furaha, hakuna kitu cha kushikika kinachoweza kutupatia furaha hiyo, kwa ambaye ameelewa maana halisi ya uwepo wetu hapa duniani..
Mada nyingine ya kupendeza kwa Wastoiki ilikuwa hasira. Warumi walikuwa na tabia ya hasira. Wastoiki walitaka kuwatuliza lakini walifanya hivyo kwa njia isiyo ya kawaida kupitia hoja za kiakili. Walipendekeza kuwa, kupata hasira si kitu unachofanya kwa sababu eti una tabia flani ya asili, au kwamba damu inachemka basi ni rahisi kukasirika. Waliona hasira ni kama matokeo ya kuwa mjinga, kuwa na mawazo yasiyo sahihi kuhusu maisha. Hasira inatokea pale ambapo matumaini yasiyofaa yakigongana na uhalisia usiyotarajiwa.
Hatuwezi kupiga kelele kila wakati kitu kibaya kinapotokea kwetu, bali tunapopiga kelele ni wakati tu kitu hiko ni kibaya na hakijatarajiwa. Kwa mfano, hutaweza kupiga kelele kwa sababu tu mvua imeanza kunyesha, ingawa mvua inaweza kuwa mbaya na ikakuharibia siku yako lakini kwa sababu umejifunza kutarajia mvua basi utaona ni kawaida. Vivyo hivyo inapaswa kuwa kwenye kila kitu: usitarajie mvua tu, tarajia usaliti, ukatili, wizi, aibu, tamaa, chuki, maradhi, kufeli n.k. Mtu ataacha kuwa na hasira sana endapo tu atajifunza ukweli wa maisha ya mateso. Mtu mwenye busara anapaswa kujitahidi kufikia hali ambayo hakuna kitu chochote kinachoweza ghafla kuvuruga amani yake ya akili. Kila janga linapaswa kuwa tayari limehesabiwa, na limetarajiwa kama anavyofanya mhasibu makini.
Nittakuacha na kauli nzuri zaidi ambayo Seneca alisema wakati walinzi wa Nero walipokuwa wakimshika na kumsukuma kwenye bafu ambako alikusudiwa kuchukua kisu kikali na kujiua. Mke wake Paulina na watoto wake wawili walikuwa wakihangaika, wakilia, waking’ang’ania vazi lake. Seneca aliwageukia, akawapatia tabasamu la kuchoka na kusema kwa urahisi: "Kuna haja gani ya kulia juu ya sehemu tu za maisha? Maisha yote yanahitaji machozi." Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Wastoiki.
0 Maoni