Siku hizi, karibia kila mtu anaanzisha biashara lakini matokeo hayaonekani, idadi ya biashara zinazofanikiwa ipo chini sana. Kwenye kuanzisha biashara au kampuni ndogo tu, mana ndio mwanzo huo, ni lazima uwe miongoni mwa wafanyabiashara walio tayari kuwekeza jitihada za hali na mali, ili kuhakikisha unachokianzisha kinafanikiwa.
Kosa kubwa nililoliona ni wafanyabiashara wanaojaribu kuendeleza mtindo au kukopi kitu ambacho tayari kimefanywa.
Je! Unamfahamu mtu yeyote ambaye huwa anaanzisha biashara mpya lakini akili yake haitulii na wazo moja, na biashara inaishia kufeli ?
Sababu ya kufeli huku ni kujaribu kutengeneza pesa wakiwa na fikra kwamba pesa pekee itawaletea furaha - kama msemo wa kawaida unavyosema, pesa haileti furaha, yaah ni hivyo.
Pesa itakutatulia matatizo yanayohitaji pesa, ila sio chanzo cha furaha. Ikiwa utachagua kujitahidi kujenga kampuni ndogo inayofanikiwa, basi lazima uchague tasnia au sekta ambayo unapenda na upo tayari kubobea katika kitu hicho.
Kwa maneno rahisi, ushauri huu bora zaidi ni kwamba fikiria ni nini unachofanya maishani mwako ambacho kinakufanya uwe na furaha sana. Kitu chochote ambacho ni hicho kimoja, ndicho unachopaswa kuanzisha biashara iliyojikita katika kitu hicho iwe moja kwa moja, au inahusiana na hiko kitu.
Binafsi, kuna vitu vingi ambavyo nina shauku navyo, lakini kitu pekee kinachonipa amani sana ni hali ya kuwavutia watu na kusambaza elimu yoyote niliyonayo, naweza kujiita mwanafunzi wa maisha, lakini pia unaweza kusema mwalimu japo sikuikubali kazi ya ualimu, ninapopata nafasi ya kumuelewesha mtu jambo, najisikia kama nipo juu ya ulimwengu na kana kwamba hakuna kitu kinaweza kunizuia. Na ni katika wakati huu nina uhakika ninaweza kupata kipato kupitia stadi yangu hii.
Kwa hiyo, baada ya kusema hayo yote, hapa chini kuna njia tatu za kufanikiwa katika biashara au kampuni yoyote ndogo unayoanzisha.
1. Tengeneza mtandao imara wa watu.
Unapoanza biashara kutoka mwanzo, unahitaji mtandao wa watu ambao unaweza kuwaleta katika biashara au kampuni yako, au ambao wanaweza kusaidia kusambaza habari kuhusu kampuni yako. Ikiwa hii ni biashara yako ya kwanza, basi kuna uwezekano mkubwa utakuwa na orodha ndefu ya watu uliowahi kufanya nao kazi au kushirikiana nao kwa kiwango fulani katika pendekezo/wazo la biashara au kampuni tofauti kabisa.
Watu hawa ni muhimu sana kwenye mafanikio ya kampuni yako. Acha kufikiria kwamba unapaswa kujaribu kuwauzia bidhaa zako watu hawa ambao ulikuwa unawajua wakati ulipokuwa unafanya kazi yako ya zamani au ni marafiki zako tu. Ingawa unaweza kuwauzia baadhi yao, unahitaji kuwafikiria watu hawa kama watu wanaoweza kukufungulia milango ya kuongeza wigo wa biashara yako.
Wanaweza wasinunue moja kwa moja bidhaa au hudumazako, lakini watakuelekeza kwa watu wanaoweza kununua kutoka kwako. Ili hii ifanye kazi, ni muhimu kufuata njia sahihi. Ikiwa unakutana na watu wako wa karibu, watu walio kwenye mtandao wako na wakahisi kama unataka tu kuwauzia, basi utawakatisha tamaa watu hawa kwenye kukupatia msaada.
Wakati huo huo, ni muhimu kuwauliza wengine wanachokifanya kama wana biashara zao, au laah jaribu kubaini kitu chochote ambacho wanakwama katika maisha yao ya kila siku na kuona ikiwa unaweza kuwasaidia kwa namna yoyote ile. Mara nyingi, binafsi huwa naona njia bora naweza kuwasaidia ni kwa kuwakutanisha na mtu anayeweza kuwa na thamani kwao.
Watu wana matatizo mengi kama vile nidhamu, ubunifu, afya na mazoezi na mengine chungu nzima.
Licha ya maneno haya kuwa rahisi sana, usidharau nguvu ya mbinu hii.
2. Maono (Vision) yako yawe yenye kujali hisia za watu.
Nimesikia mara nyingi kwamba, “tengeneza maono ambayo yanavutia." Hii ni kweli, lakini jambo ambalo watu wanalisahau ni kwamba pia yanahitaji kuwa yenye kubeba hisia za watu, maono (vision) yako iwe imebeba mambo ambayo wengine wameyaweka karibu kabisa na mioyo yao. Mfano mabadiliko ya tabia nchi ni jambo ambalo linavutia kulifahamu na kulizuia, lakini kwa watu wengi, hiko sio kipaumbele kabisa.
Ila mfano ungesema maono yako ni "kuboresha lishe ya jamii yetu ya waTanzania" kungekuwa na kikundi cha watu ambao kidoogo wangekufikiria. Kadri biashara yako inavyobeba maono ambayo watu wanayajali, ndivyo unaongeza uwezekano wa kupata soko kubwa zaidi .
Usidharau thamani ya masoko madogo madogo. Hata kama soko la bidhaa au huduma husika ni dogo sana, kuna fursa ya matawi kwenye soko hilo, kwa maana ya masoko madogo madogo ambayo hayahudumiwi na mtu yeyote. Ikiwa unaweza kupata kona yako moja ambayo haihudumiwi na watu na ambayo wahusika wanaijali, basi una wazo la biashara au kampuni ndogo ambayo ina nafasi ya kufanikiwa.
Mfano, kama wewe unatoa huduma za graphics designing basi unaweza ukatumia ujanja kidogo kwa kusema unahudumia wanawake wenye biashara ndogo ndogo kwa kuwatengenezea graphics kwa bei rahisi, ni uhakika kuwa hawa watakuletea wengine. Na si kwamba hautapata wateja wanaume, lazima utawapata. Hii ndio nguvu ya kujichagulia soko dogo na kulitawala.
3. Fanya Utafiti wa Kina na Pia Jaribu Wazo Lako.
Jambo moja ambalo nimeona biashara pamoja na kampuni nyingi ndogo zinafanya ni kuingia sokoni na wazo ambalo linakidhi mahitaji yao wanayohisi ni tatizo la kila mtu. Ingia nalo ulingoni kwa raia kulijaribu, na hapo ndio utajua kama lina manufaa.
"Endapo unafikiria kwamba kitu fulani ni cha thamani, haimaanishi kuwa watu wengine watafikiria vivyo hivyo kama wewe, ondoa hii dhana."
Ushauri muhimu naweza kutoa ni kuhakikisha kila wakati kabla ya kuanza unalijaribu soko lako, lakini hapa ndipo kuna tatizo; watu wanafikiria unahitaji mamilioni ya watu - Laaah. Nimeona mifano mingi ambapo wahusika wanajaribu bidhaa zao miongoni mwa watu kadhaa na kupata mrejesho wa uhakika.
Kwa hivyo, ikiwa watu 100 wanapenda wazo lako, kuna nafasi kubwa kuwa unaelekea kwenye njia sahihi. Hakikisha tu kuwa watu hao100 sio marafiki zako wote, vinginevyo maoni yao yatakuwa na upendeleo kwa sababu mnafahamiana.
Pia kama wewe ni mwanzilishi wa biashara au kampuni ndogo, usione tabu kukaa na wateja au wateja watarajiwa, bila kuwaambia kuwa wewe ndo mmiliki. Hii inaweza kukupatia ufahamu mzuri wa soko husika ambao utakusaidia katika hatua za majaribio, lakini pia kujua wapi pa kuboresha.
0 Maoni