The 48 Laws of Power

 



Kitabu cha 48 Laws of Power kilichoandikwa na mwandishi mahiri wa karne hii Robert Greene.

"The 48 Laws of Power" ni kitabu kilichoandikwa na Robert Greene kuhusu "sheria" ambazo watu wenye nguvu, mamlaka na madaraka katika historia wametumia kuzipata pamoja na kudumu na nguvu zao. Katika kitabu hicho, Robert Greene anadai kwamba binadamu hatuwezi kujiondoa kwenye mchezo huu wa kutafuta ukuu, madaraka  na nguvu juu ya wengine, hivyo ni bora zaidi kuwa mchezaji mwenye ujuzi kwa kujifunza sheria na mikakati iliyotumiwa tangu zamani na inaendelea kutumika hadi leo.

Binadamu hatuwezi kuvumilia kutokuwa na nguvu. Kila mtu anataka nguvu na madaraka juu ya wengine na kila nafasi tunayopata atunajaribu kupata zaidi. Kupigania na kutumia nguvu hizi ni mchezo ambao kila mtu anaushiriki, iwe utataka au la, hivyo unaweza kuwa mchezaji mahiri au kibaraka tu ambaye watu wengine wanakutumia kutimiza azma zao.

Kwa hiyo, kitabu cha "The 48 Laws of Power" kinahusu nini ? 

Greene ameandika sheria 48 za nguvu kulingana na mifano na historia za watu waliofanikiwa au kushindwa kutumia nguvu ipasavyo, na mwisho wakapata matokeo ya kuvutia au ya yasiyoridhisha. Greene analeta hoja kwamba kufuata sheria hizo 48 kwa ujumla kutakuongezea nguvu, wakati kushindwa kuzifuata kutapunguza nguvu yako, au hata kuirudisha nyuma. Anatoa maelezo kuhusu jinsi ya kutumia sheria hizo, pamoja na mifano na uchambuzi lakini nitoe angalizo kuwa baadhi ya sheria hizi haziendani na malezi pamoja na makuzi yetu,, lakini haidhuru kuzitambua kwa sababu ufahamu wako juu ya sheria hizi utakuwezesha kujilinda endapo kuna watu watataka kuzitumia dhidi yako.

VIDOKEZO MUHIMU
Kwa kuwa sheria 48 zina urefu kiasi, nimejaribu kuangalia sheria ambazo zinaendana na kuzijumuisha pamoja iwe kama summary nyepesi ya kukupa uelekeo, endapo kuna haja ya kuimarisha uelewa wako kwenye nyanja husika.

1. Kuwa makini na binadamu na elewa tabia zao, ikiwemo za kwako mwenyewe (Sheria 19 na 33)

  • Vitendo, Ishara, na Hisia zina nguvu zaidi kuliko maneno (Sheria 9, 27, 32, 37 na 43).
  • Kujali maslahi yako mwenyewe ni kichocheo kinacholeta msukumo zaidi kuliko kutarajia huruma au shukrani nyingi kwa watu baada ya msaada (Sheria 13). Kushukuru ni mzigo ambao watu watataka kujitua nao muda wote (Sheria 2 na 16).
  • Jihadhari na Wivu kwa kuwa ni hatari, na jinsi unavyopaswa kuwa makini nao (Sheria 1, 2 na 46).
  • Thamani ya kitu huongezeka kinapokuwa adimu - watu wanataka vitu ambavyo hawawezi kuwa navyo (Sheria 16.
  • Watu wanapenda ukale na hawapendi mabadiliko mengi au ya ghafla (Sheria 45.
  • Hisia na hali ya watu wanaotuzunguka ina mchango mkubwa sana kwenye kuathiri tabia zetu (Sheria 10).
  • Nguvu huwa mikononi mwa watu wachache kwenye kundi la watu (Sheria 42)
  • Kuchanganya na kuwavuruga wengine kunakupa nafasi ya kufanya mambo yako kwa usiri (Sheria 6, 12, 37 na 44).

2. Kuna muda muonekano wa mambo una nguvu zaidi kuliko ukweli (Sheria 50)
  • Unaweza kupata nguvu kwa kuwa mkweli juu ya ujuzi wako au kuigiza tu kwamba una ujuzi fulani (Sheria 7, 11, 26 na 30), au kujiwekea hali ya utata ambayo itafanya watu iwe ngumu kukutambua (Sheria 3, 4, 6, 16 na 17), au kuondoa hali ya ukawaida (Sheria 34 na 36).
  • Unaweza kuonekana dhaifu kwa kuwa na hasira au kuwa na jazba juu ya vitu ambavyo huwezi kuwa navyo (Sheria 36), au kulingwanishwa na mtu ambaye amekuzidi (Sheria 41).
  • Kuna hasara kwenye kuonekana bora na mkamilifu sana kuliko wengine, hii itafanya wakuone tishio (Sheria 1, 18 na 46). Kuna muda ni vyema kuonekana dhaifu ili wengine wasitishike na uhalisia wako (Sheria 21 na 22)
  • Kuna wakati ni vyema kuwa tofauti (Sheria 6 na 37) lakini kuna wakati inabidi uigize kuwa sawa na wengine wanaokuzunguka (Sheria 3, 38 na 44)

3. Taarifa ni muhimu sana
  • Kuwa na habari za watu wengine, hasa kuhusu madhaifu yao (Sheria 14, 18, 19 na 33)
  • Usifunguke sana kwa wengine kuhusu maisha yako (Sheria 3, 4 na 17)

4. Weka mipango na fikiria kuhusu mbinu tofauti tofauti (Sheria #29), lakini pia kuwa na uwezo wa kubadilika (Sheria 20, 24, 38, 44 na 48).
  • Kuwa mwongozaji badala ya kuwa mpokeaji (Sheria 8, 25, 28, na 31)
  • Kuvuruga mipango ya wengine kunaweza kuwa na manufaa kwako (Sheria 8, 28 na 39)
  • Kuwa na subira na ona mbali zaidi ya wengine (Sheria 22, 29 na 35)

5. Tumia mantiki zaidi na sio hisia kwenye kufanya maamuzi (Sheria 2, 39 na 47), na epuka kuyumbishwa (Sheria 36 na 40)

6. Onyesho kubwa la nguvu linaweza kuwa muhimu nyakati fulani (Sheria 15, 23 na 28) lakini mara nyingi ni bora kutumia ukimya na kuficha uhusika wako (Sheria 11, 24, 31, 43 na #44)
Kufikia hapa, ninahitimisha utangulizi wa makala hii ambayo itakuwa na muendelezo wa makala zitakazochambua sheria za kwenye kitabu hiki, kila makala inayofuata itakuwa na uchambuzi wa sheria angalau tatu (3) ambapo utapata funzo la sheria husika, KAA MKAO WA KULA.
Maisha Max pia inapatikana kwenye mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, telegram, youtube pamoja na blog hii ambayo imesheheni machapisho kadha wa kadha ya kukuelimisha juu ya mambo mbalimbali ya faida kwa maisha yako.
https://t.me/maishamax - Comment hapa kwa kutumia link hii

          Chapisha Maoni

          0 Maoni